Tuesday, December 25, 2012

SAMATTA NA ULIMWENGU WAFUNGUKA JUU YA TUHUMA ZA KULINGA KUCHEZEA TAIFA STARS.



Kim Poulsen akiwatoa maelekezo kwa vijana wake Thomas Ulimwengu na mwenzake Mbwana Samatta mazoezini jijini Dar es Salaam
EDO KUMWEMBE
WASHAMBULIAJI wawili wa kimataifa wa Tanzania wanaokipiga TP Mazembe, Mbwana Samatta 'Poppa' na Thomas Ulimwengu wamevunja ukimya kuhusu madai kwamba wanaringa na wanaipuuza timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Mastaa hao walizomewa katika pambano la kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo lililopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa na Stars kushinda bao 1-0 lililofungwa na Mrisho Ngassa.

Wakiongea kwa uchungu katika nyakati tofauti juzi Jumapili, Samatta na Ulimwengu ambao kitabia ni wakimya walitoa dukuduku lao katika mahojiano maalumu waliyofanya na Mwanaspoti huku kila mmoja akionyeshwa kukerwa na kitendo cha kuzomewa na mashabiki wa soka na kusisitiza kwamba wanaonewa na mashabiki kutokana na kutoambiwa ukweli kuhusu wao.

Maelezo ya Samatta
"Kaka ukweli ni kwamba mimi naumwa ingawa Watanzania hawataki kuelewa. Niliumia bega katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tuliyocheza ugenini dhidi ya Power Dynamo ya Zambia.

Kama unakumbuka mechi ya marudiano pale Lubumbashi mimi hata sikucheza. Sasa wiki chache zilizopita tulikwenda Congo Brazzaville kucheza mechi ya kirafiki ambayo ilikuwa ni ya kuadhimisha kumalizika kwa vita nchini humo. Katika mechi nikajitonesha bega na mpaka sasa linanisumbua sana," anasema Samatta.

"Mwalimu (Kim Poulsen) nimeongea naye sana na amenielewa. Ameniambia mimi ni kijana mdogo kwa hiyo nikipata tatizo niliseme kwa haraka.

Na ametuambia mimi na Thomas kuwa kwa sababu sisi ni majeruhi basi tutaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Daktari Mwankemwa.

Hivi ninavyokwambia sasa hivi naenda katika shamba la baba kule Vikindu kula embe, ikifika saa sita inabidi nirudi niende kwa Daktari Mwankemwa kufanya naye mazoezi.

Januari 6, mwakani tunahitajika katika kambi ya timu ya taifa. Kim kaniambia kuna mechi tatu za kirafiki.

Nikiwa fiti nacheza kama kawaida. Siwezi kucheza wakati sipo fiti jamani.

Nikicheza wakati siko fiti huwa nacheza kwa kiwango cha chini na watu wanasema mimi sio mzalendo, nikikaa nje kupisha watu walio fiti wanasema mimi sio mzalendo, sasa nifanyeje?� alihoji Samatta.

�Mechi yetu ya Zambia ilikuwa ya kirafiki tu, lakini si unakumbuka kuna mechi za maana kibao zinakuja? Inabidi niwe fiti.

Watu wamekasirika kwa sababu tumeikosa Zambia, lakini kuna mechi za Morocco, Ivory Coast ni muhimu sana kuliko hii ya Zambia.

Samatta pia alitoa angalizo kwa TFF kuwa tarehe ambazo Stars itaingia kambini wao wanatakiwa kurudi Lubumbashi kwa hiyo ni bora wawasiliane na timu yao ya TP Mazembe.

"Sisi tunahitajika Lubumbashi kati ya tarehe 7 hadi 10. Lakini kambi ya timu ya taifa itakuwa Januari 6. Kwa hiyo hapo TFF lazima wapeleke taarifa Mazembe kwa sababu tunaweza kuharibu kule au huku tukaonekana wabaya," aliongeza Samatta.

Kuhusu kukosekana kwao katika michuano ya Chalenji kule Uganda, Samatta anajitetea kwa kusema; �Mazembe walitunyima ruhusa. Hatuwezi kutoroka kambini jamani.

Walisema hawaitambui michuano hiyo kwa sababu haiko katika ratiba ya Fifa. Sisi tungefanya nini jamani?

Kuhusu kuzomewa na mashabiki, huku shabiki mmoja akiwa ana bango lililoandikwa "Who needs Samatta, We have Ngassa", Samatta anadai kwamba matukio hayo yameinua ari yake.

"Kuna kitu nimejifunza kwamba watu wanaipenda timu ya taifa. Hilo ni jambo zuri, lakini hawaambiwi ukweli. Na mimi naipenda sana na kila ninapoitwa huwa nakuja kasoro michuano ya Chalenji tu. Mimi sijawasikiliza kabisa walionizomea."

Maelezo ya Ulimwengu
Wakati Samatta akisema hayo, Ulimwengu ambaye alizungumza akiwa maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam, alisema hana sababu ya kuringa kwa ajili ya timu ya taifa lakini amevunjwa moyo sana na kuzomewa na mashabiki.

"Kaka mimi niliumia goti la kushoto kati ya Novemba 7 au 8 mwezi uliopita.

Hata wewe nadhani nilikwambia kabla hata hizi habari za kuitwa na timu ya taifa. Nitakutumia picha uone wakati natibiwa na daktari wa Mazembe ninazo katika laptop yangu, anasema Ulimwengu.

'Hata katika mechi hiyo ya kirafiki ambayo Samatta anasema Mazembe ilikwenda Brazzaville mimi niliachwa niendelee na matibabu.

Siwezi hata kufanya mazoezi na Daktari wa Mazembe aliniambia nikae nje kwa wiki tatu na nianze kufanya mazoezi mepesi mwishoni mwa wiki hii," anasema Ulimwengu.

"Nimesikitika sana kuzomewa lakini mimi ni mzalendo damu. Nimecheza katika mechi zote za timu ya vijana na wote mnajua. Sasa kwa nini niache kucheza leo? Nimesikitika sana kuzomewa na roho inaniuma sana kwa sababu watu wanapotosha ukweli.

"Kocha Kim nimeongea naye na amenielewa sana. Tatizo mashabiki na waandishi hawaelewi kwa sababu hatujawahi kuongea.

Mimi nimewahi kutoka Ulaya kwa ajili ya kuichezea timu ya vijana sasa nitashindwa vipi kuichezea timu ya taifa nikitokea hapo Congo tu," aliongeza Ulimwengu.

Ulimwengu amesema akiitwa tena katika timu ya taifa atacheza kwa nguvu zake zote na kuwanyamazisha mdomo wale wote waliomzomea Jumamosi jioni.

"Mimi mzalendo na nitawaonyesha kwa kucheza kwa juhudi. Waliotuzomea mimi na Samatta wametuharibia sana na vyombo vya habari bado havijatafuta ukweli sana zaidi ya kutuchafua," alisema Ulimwengu.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...