Monday, November 19, 2012

AJIRA: Walimu wote waliomaliza vyuo kuajiriwa



SERIKALI imetangaza kuajiri walimu wote watakaomaliza vyuo mwaka huu kuanzia Januari 2013.
Akizungumza kwenye mahafali ya nne ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (MUCE) kilichopo Manispaa ya Iringa, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo alisema zaidi ya nusu ya ajira za mwaka wa fedha 2012/13 ni za walimu.
Alisema ajira za mwaka huu ni 56,678 zinazojumuisha sekta zote lakini kwa walimu ni 28,638 ambazo ni zaidi ya idadi ya walimu wote wanaomaliza vyuo mbalimbali mwaka huu.
Mulugo alisema walimu watakaoajiriwa watapelekwa kwenye halmashauri na si mijini wala kwenye majiji kutokana na wengi wao kukimbia maeneo ya vijijini.
“Tumeamua kuwapeleka walimu maeneo ya vijijini ili kutatua tatizo la walimu huko na kutokana na utafiti tuliofanya miaka ya nyuma,” alisema.
Alisema miaka ya nyuma kuna maeneo mengi ya vijijini ikiwemo yale ya mikoa ya Kigoma, Shinyanga, Mwanza, Manyara, Mbeya, Rukwa na Katavi zaidi ya nusu ya walimu waliopangiwa huko hawakuripoti wakati wale wote waliopangiwa mijini waliripoti wote.
Aidha alisema Serikali itatoa adhabu kali kwa walimu wote ambao wamekwenda kusoma bila ruhusa kutokana na kukiuka maadili ya kazi.
Alisema wizara yake imegundua kuwa kuna walimu wengi wametoroka makazini na kwenda kusoam vyuo mbalimbali bila kupata ruhusa kutoka kwa waajiri wao ambao ni wakurugenzi wa Halmashauri.
Alisema lengo la zoezi hilo ni kuweka mambo sawa na kuwa na walimu waadilifu na wenye moto wa kufanya kazi na kuwa adhabu hizo ni pamoja na kukata mishahara yao na nyingine zitatolewa kulingana na taratibu za kazi na adhabu za utumishi.
Alisema pia kuna changamoto nyingine inayojitokeza ya walimu waliosoma kutaka kubadilishiwa vituo vya kazi au kupata vyeo ikiwemo kutoka shule za msingi kwenda sekondari na kutoka walimu wa kawaida kuwa maafisa elimu.
Alisema Serikali haijawatuma wasome ili wawe maafisa elimu na kusoma si kigezo cha kuwa na cheo hicho na kwamba huko huko wanakofundisha iwe shule za msingi au sekondari wanahitaji walimu wenye uelewa na ujuzi.
Kwenye mahafali hayo ya nne jumla ya wahitimu 703 wakiwemo wanaume 378 na wanawake 325 wa fani za elimu za sayansi za jamii na ualimu, sayansi ya jamii 30 sayansi na ualimu 108 na elimu katika sayansi 23.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...