Monday, November 26, 2012

Ridhiwan, Lowassa waelezea utajiri wao

 
Ridhiwan Kikwete 

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan wamezungumzia tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwao kwamba wanamiliki rasilimali zenye thamani ya mabilioni ya shilingi.
Lowassa kwa upande wake amekuwa akidaiwa kuwa tajiri anayemiliki kampuni kubwa za kibiashara na kumekuwa na taarifa kwamba ana ukwasi ambao vyanzo vyake vinatia shaka na siyo rahisi kuvitolea maelezo.
Kwa upande wake Ridhiwan naye amekuwa akidaiwa kuwa na utajiri mkubwa na amekuwa akihusishwa na biashara za kampuni za kusafirisha mafuta ambayo hupelekwa kwenye migodi, umiliki wa hoteli na majengo kadhaa ya kifahari.
Wote wawili wamekuwa wakidaiwa kwamba baadhi ya mali zao wamekuwa wakiziendesha chini ya kivuli cha wafanyabiashara wengine wakubwa nchini ili kukwepa kuhojiwa walikotoa utajiri huo, taarifa ambazo hata hivyo imekuwa vigumu kuzithibitisha.
Hata hivyo jana kwa nyakati na mazingira tofauti, Lowassa na Ridhiwan walijitokeza hadharani na kukanusha madai kwamba wao ni matajiri wa kupindukia.
Lowassa kwa upande wake akiwa mjini Mbeya alisema yeye siyo tajiri kama ambavyo imekuwa ikidaiwa lakini wakati huohuo akasema “sijafilisika”.
“Wengi wanasema kuwa mimi ni tajiri siyo kweli, lakini sijafilisika kutokana na kuchangia makanisa kwani nina marafiki wengi ambao wananisaidia katika kuchangia makanisa nao pia hawajafilisika,”alisema Lowassa.
Lowasa alitoa kauli hiyo alipokuwa akiendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa hosteli ya wanachuo wanawake ambao ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Theofilo Kisanji cha mkoani Mbeya, kinachomilikiwa na Kanisa la Moraviani Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi.
Kiongozi huyo ambaye alichangia kaisi cha Sh25 milioni, alisema kila mtu ana wajibu wa kuchangia elimu na kwamba mwanamke anapaswa kutazamwa kwa karibu zaidi kwani ndiye anayebeba jukumu kubwa la kutunza familia.
Kwa upande wake Ridhiwan alisema: “Ikiwa mimi ni tajiri wa kiasi kinachosemwa, basi mimi ninamzidi Bakhressa (Said Salim, mfanyabiashara maarufu Afrika Mashariki), maana nimepewa kila hoteli hapa mjini, kampuni za mafuta na kila biashara kubwa inayoanzishwa hapa mjini ni ya Ridhiwan”.
Said Salim Bakhressa ni mfanyabiashara ambaye anatajwa kuwa tajiri kuliko wote nchini na anashika nafasi ya pili katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku akiwa miongoni mwa wafanyabiashara 10 wanaonyemelea kuingia katika nafasi za juu za utajiri Afrika.
Hata hivyo Ridhiwan ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), aliongeza: “Ninaweza kuwa nafanya biashara moja au mbili, lakini siwezi kuwa mmiliki kiasi chote hicho cha mali.
Mtoto huyo wa Rais Kikwete alikuwa akijibu tuhuma kwamba magari yake kumi ya kusafirisha mafuta yamekamatwa na kuzuiwa katika mpaka wa Kenya na Tanzania, Namanga mkoani Arusha kutokana na kukwepa kodi, taarifa ambayo aliikanusha.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...