WAKATI matokeo ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), yakiwa yamevuja baadhi ya wapambe wa wagombea walioshinda wameanza kusherehekea, huku wengine wakitambiana.
Hata hivyo, matokeo hayo yamekuwa machungu kwa baadhi ya vigogo walioanguka wakiwamo mawaziri, wabunge na watu maarufu.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuunda sekretarieti mpya baada ya uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar utakaofanyika leo.
Kwa upande wa Zanzibar, matokeo hayo yanaonyesha kuwa walioshinda ni pamoja na Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif Khatib; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Fedha Zanzibar, Omar Yussuf Mzee, Abdulhakim Chasama na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha.
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Khadija Hassan Aboud, Bhaguanji Mansuria, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Khamis Mbeto.
Watu maarufu walioangukia pua katika uchaguzi huo ni Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Abdallah Juma Sadallah, mtoto wa Rais Mstaafu, Abdallah Mwinyi ambaye pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Mbunge wa Viti Maalumu, Kidawa Salehe na Naibu Waziri wa Fedha wa zamani, Abdisalaam Issa Khatib.
Walioshinda Bara
Majina ya wajumbe wa Nec walioshinda bara na kura walizopata katika mabano ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira aliyeongoza kundi hilo kwa kupata kura 2,135, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (2,093), Mwekahazina wa CCM, Mwigulu Nchemba (1,967), na Katibu wa UVCCM, Martine Shigela (1,824).
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi (1,805), Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe (1,455), Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo (1,414), Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome (1,207), Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama (1,174) pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Fenela Mukangara (984).
Wakati walioshinda Bara na wapambe wao wakitambiana, majina makubwa yaliyoanguka katika uchaguzi huo ni pamoja ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama, Richard Hiza Tambwe na Mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini, Ruth Msafiri.
Wassira atajwa kumrithi Mkama
Habari zilizopatikana jana mjini hapa zinaeleza kuwa Wassira, anatajwa kuwa anaweza kuikwaa nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho.
Wengine wanaotajwa kuwa wanaweza kupata nafasi hiyo ya Katibu Mkuu ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye pamoja na Waziri Lukuvi.
Makundi yatambiana
Tambo na kejeli za wapambe, jana zilitawala katika viwanja vya Ukumbi wa Kizota unakofanyika Mkutano Mkuu wa CCM, baada ya baadhi ya wajumbe kuanza kusherehekea kutokana na kupata matokeo.
Nje ya ukumbi huo, tangu asubuhi wapambe wa wagombea hao walionekana wakiwa wamekaa katika makundi huku wakinunuliana vinywaji.
Ingawa matokeo yalitarajiwa kutangazwa leo, lakini takriban wajumbe wote wa mkutano huo walionekana kuyapata hali ambayo iliwafanya walioshinda kupongezwa wakati wakiingia katika ukumbi wa mikutano.
Mwananchi lilimshuhudia, Waziri Mathayo akipongezwa na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo nje ya ukumbi wa mkutano asubuhi.
Pamoja na kupongezwa na wajumbe wa mkutano huo hata washindi wa uchaguzi huo nao walipokutana walipongezana.
Mwananchi lilimshuhudia, Shigela akimpongeza Waziri Wassira na baadaye walikumbatiana na kupongezana na Nchemba. Baadaye baadhi ya wajumbe walimbeba Shigela juu juu wakimpa pongezi.
Wakati Shigela akibebwa, baadhi ya wajumbe walimfuata Wassira na kumpongeza kwa kumshika mikono na wengine kumkumbatia huku yeye wenyewe akitamba kuwa ni mwarobani wa Chadema.
Waziri Membe akiwa ndani ya ukumbi wa mkutano, baadhi ya wajumbe wanaomuunga mkono walimfuata na kumzunguka huku wengine wakimkumbatia.
Walioanguka watoweka
Wakati walioshinda wakionekana kufurahi na kupongezwa, hali ilikuwa tofauti kwa wagombea walioshindwa, kwani baada ya kupata matokeo hayo wengi walitoweka katika eneo la ukumbi huo.
Kamati ya Uchaguzi yalala ukumbini
Kamati iliyokuwa ikisimamia uchaguzi huo jana ililala katika ukumbi wa kuhesabia kura kutokana na kazi hiyo kumalizika usiku wa manane, huku baadhi ya watu waliokuwa wakifanya kazi hiyo kunyang’anywa simu zao ili matokeo yasivuje.
Watu hao waliondoka katika ukumbi wa kuhesabia kura uliopo katika Ukumbi wa Kizota saa 12:00 asubuhi.
No comments:
Post a Comment