SERIKALI imetangaza kuajiri walimu wote watakaomaliza vyuo mwaka huu kuanzia Januari 2013.
Akizungumza kwenye mahafali ya nne ya Chuo Kikuu
Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (MUCE) kilichopo Manispaa ya Iringa,
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo alisema zaidi
ya nusu ya ajira za mwaka wa fedha 2012/13 ni za walimu.
Alisema ajira za mwaka huu ni 56,678
zinazojumuisha sekta zote lakini kwa walimu ni 28,638 ambazo ni zaidi ya
idadi ya walimu wote wanaomaliza vyuo mbalimbali mwaka huu.
Mulugo alisema walimu watakaoajiriwa watapelekwa
kwenye halmashauri na si mijini wala kwenye majiji kutokana na wengi wao
kukimbia maeneo ya vijijini.
“Tumeamua kuwapeleka walimu maeneo ya vijijini ili
kutatua tatizo la walimu huko na kutokana na utafiti tuliofanya miaka
ya nyuma,” alisema.
Alisema miaka ya nyuma kuna maeneo mengi ya
vijijini ikiwemo yale ya mikoa ya Kigoma, Shinyanga, Mwanza, Manyara,
Mbeya, Rukwa na Katavi zaidi ya nusu ya walimu waliopangiwa huko
hawakuripoti wakati wale wote waliopangiwa mijini waliripoti wote.
Aidha alisema Serikali itatoa adhabu kali kwa
walimu wote ambao wamekwenda kusoma bila ruhusa kutokana na kukiuka
maadili ya kazi.
Alisema wizara yake imegundua kuwa kuna walimu
wengi wametoroka makazini na kwenda kusoam vyuo mbalimbali bila kupata
ruhusa kutoka kwa waajiri wao ambao ni wakurugenzi wa Halmashauri.
Alisema lengo la zoezi hilo ni kuweka mambo sawa
na kuwa na walimu waadilifu na wenye moto wa kufanya kazi na kuwa adhabu
hizo ni pamoja na kukata mishahara yao na nyingine zitatolewa kulingana
na taratibu za kazi na adhabu za utumishi.
Alisema pia kuna changamoto nyingine inayojitokeza
ya walimu waliosoma kutaka kubadilishiwa vituo vya kazi au kupata vyeo
ikiwemo kutoka shule za msingi kwenda sekondari na kutoka walimu wa
kawaida kuwa maafisa elimu.
Alisema Serikali haijawatuma wasome ili wawe
maafisa elimu na kusoma si kigezo cha kuwa na cheo hicho na kwamba huko
huko wanakofundisha iwe shule za msingi au sekondari wanahitaji walimu
wenye uelewa na ujuzi.
Kwenye mahafali hayo ya nne jumla ya wahitimu 703
wakiwemo wanaume 378 na wanawake 325 wa fani za elimu za sayansi za
jamii na ualimu, sayansi ya jamii 30 sayansi na ualimu 108 na elimu
katika sayansi 23.
No comments:
Post a Comment