MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Geita wametofautia na madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Geita vijijini kuhusiana na mgawanyo wa mrabaha wa madini wa dola 200,000 za Marekani unaotolewa na Kampuni ya uwekezaji ya Mgodi wa dhahabu wa Geita[GGM] kila mwaka.
Hatua hiyo imekuja kutokana na madiwani hao
kuonyesha msimamo wao kwa kuitaka halmashauri ya Geita Vijijini kuacha
kuingilia rasilimali zilizomo ndani ya Mji wa Geita ikiwemo fedha
inayotolewa na GGM.
Madiwani hao kupitia kikao cha baraza
kilichofanyika Novemba 16,mwaka huu katika ukumbi wa GEDECO walisema
haiwezekani fedha inayotokana na mrabaha wa madini ikagawiwa kwa
asilimia sawa wakati asilimia 100 ya Mgodi wa Geita umo ndani ya
halmashauri ya mji wa Geita.
Msimamo wa madiwani hao umekuja siku chache baada
ya kuvunjwa kwa iliyokuwa halmashauri ya Wilaya ya Geita na kuanzishwa
halmashauri hizo mbili ambapo katika kikao cha hivi karibuni madiwani
hao walishindwa kuelewana kuhusu mgawanyo huo.
Hatua hiyo ilimfanya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Said
Magalula kuingilia kati na kuwataka madiwani hao waliovutana kwa muda wa
saa moja,kuunda kamati ndogo ya kufuatilia takwimu na mipaka halisi ya
Mji wa Geita, kauli iliyoungwa mkono na madiwani hao na hivyo kulazimika
kuwateuwa madiwani sita na wataalamu wa wilaya na mkoa kufuatilia suala
hilo.
Mvutano huo wa madiwani uliibuka Novemba 7,mwaka
huu muda mfupi baada ya Ofisa Utumishi, Charles Kimaro kusoma taarifa ya
mgawanyo wa rasilimali ya mgodi,ambapo taarifa hiyo ilionyesha kwamba
asilimia 70 ya mrabaha wa madini unabaki halmsahuri ya Wilaya ya Geita
vijijini na asilimia 30 unabaki Halmashauri ya Mji wa Geita , licha ya
mgodi huo kuwa ndani ya Mji wa Geita kwa asilimia 100.
Madiwani hao wa mji wamedai kutokuwa na imani na
kamati hiyo iliyoundwa ambayo wameitilia mashaka kuwa huenda ikapindisha
ukweli halisi wa mgawanyo wa mrabaha huo kwa kuwa halmashauri ya Geita
Vijijini ina nguvu na ina watalaamu waliobobea.
Diwani wa kata ya Mtakuja ,Hirolius Buchuma alitoa
angalizo kwa madiwani wenzake na kuomba suala hilo lijadiliwe kisheria
ili kutenda haki kwa pande zote mbili za halmashauri hizo,huku diwani wa
viti maalumu, Zaituni Fundikira akiweka msimamo wake kwamba rasilimali
zote za mji wa Geita zinabaki katika mji huo.
Kauli hiyo ya Fundikira iliungwa mkono na
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Geita, Martine Kwilasa ambaye
alisema mrabaha huo wa madini unabaki katika mji wa Geita na kuongeza
kuwa hata rasilimali zingine zilizomo ndani ya mji huo zifuatiliwe
kuhahakikisha zinabaki mikononi mwa mji huo.
Msimamo huo ulitokana na mjadala wa madiwani baada
ya mkurugenzi, Margareth Nakainga kuwasilisha taarifa ya mgawanyo wa
mali zilizokuwa zikimilikiwa na iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita
ambapo madiwani hao walidai kuwa hawakutendewa haki katika mgawanyo huo
mbali na kubaini kwamba kati ya magari 27 yaliyokuwapo wametengewa
magari 4 ambayo wamedaiwa hayakidhi utendaji wao.
No comments:
Post a Comment