KUNA kila dalili kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amekirejesha chama hicho katika mikono ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, baada ya kuwateua katika nafasi za juu za CCM waliokuwa wasaidizi wa mtangulizi wake huyo.
Wasaidizi hao ni pamoja na Makamu Wenyeviti,
Philip Mangula (Tanzania Bara) na Dk Ali Mohamed Shein (Tanzania
Zanzibar) pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, ambao
walichaguliwa na kuteuliwa katika vikao vya juu vya CCM vilivyomalizika
hivi karibuni mjini Dodoma.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa
wanasema kwamba lengo la mabadiliko yaliyofanywa ni kujaribu kurejesha
utaratibu wa CCM kuisimamia Serikali, utamaduni ambao ni kama ulikuwa
umekufa, tangu Serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani.
Mhadhiri wa zamani wa Chuo cha Ushirika Moshi,
Akwiline Kinabo anasema kwamba kuna kila dalili kuwa Mkapa ana ushawishi
katika uteuzi wa safu mpya katika sekretarieti ya chama hicho.
“Inawezekana Mangula, Kinana na Dk Shein walifanya
vizuri sana enzi za Mkapa hadi akashawishi waingizwe kwenye
sekretarieti ya sasa, lakini enzi za Mkapa na sasa ni kama mlima na
kichuguu,” alisema.
Kinabo ambaye katika uchaguzi wa CCM uliomalizika
mwezi uliopita aligombea Nec kupitia Moshi Mjini na kushindwa, alisema
viongozi hao hawawezi kwenda na kasi ya siasa za vijana wa sasa.
Kada huyo wa CCM alihoji, ”Hivi Kinana au Mangula
wataweza kushindana na hoja za Halima Mdee na Zitto Kabwe majukwaani?
Kuna vijana wengi wameshinda Nec kwa nini wasiingizwe huko?”
Naye mwasisi wa CCM na kada wa siku nyingi wa
chama hicho, Steven Mashishanga alisema kuwa viongozi waliochaguliwa
waliwahi kufanya vizuri siku zilizopita, hivyo hakuna shaka kwamba
watarejesha utaratibu wa kutekeleza mwongozo wa chama wa 1981.
“Ukisoma mwongozo huo kuanzia ibara ya 81 utabaini
kwamba kazi ya chama ni kuisimamia Serikali, hili lilikuwa halifanyiki
kwa muda mrefu katika awamu ya nne, sasa hawa waliochaguliwa lazima
waturejeshe katika msingi huo,” alisema Mashishanga ambaye aliwahi kuwa
Mkuu wa Mikoa ya Mwanza, Tabora na Morogoro.
Hata hivyo, alisema wasiwasi wake ni iwapo uongozi
mpya utaweza kuleta mabadiliko kutokana na Halmashauri Kuu (NEC) ya
chama hicho kujaa wabunge na mawaziri ambao hawawezi kuwa na ujasiri wa
kuukosoa uongozi wa juu wa chama.
“Mimi kwangu msimamo unabaki kwamba chama ni chama na Serikali ni Serikali, huwezi kuwa chama na Serikali kwa wakati huohuo.
Sasa wewe jiulize, hivi waziri anaweza kukaa
kwenye NEC akamkosoa mwenyekiti ambaye ni Rais wake? Hapo kuna kasoro
ambayo tunapaswa kuirekebisha,” alisema Mashishanga.
No comments:
Post a Comment