Rais Jakaya Kikwete amerudisha matumaini
yaliyokuwa yamepotea baada ya kusema kwamba siyo kweli kwamba mazungumzo
kati ya Malawi na Tanzania yameshindikana. Rais alisema mgogoro huo wa
mpaka katika Ziwa Nyasa hautapelekwa katika jopo la viongozi wastaafu
wanaoshughulikia migogoro ya nchi mbalimbali barani Afrika kwa
usuluhishi.
Taarifa za awali zilizokuwa zimechapishwa na
kutangazwa katika vyombo vya habari nchini zilisema mgogoro huo
ungepelekwa kwa viongozi hao wastaafu baada ya nchi hizo kudaiwa
kushindwa kuafikiana katika mazungumzo yaliyomalizika jijini Dar es
Salaam wiki mbili zilizopita na kuwakutanisha mawaziri wa mambo ya nchi
za nje wa nchi hizo mbili ambao walifuatana na maafisa wa juu wa
serikali hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe
alikaririwa na vyombo hivyo vya habari akidaiwa kusema kwamba pande zote
mbili zilikuwa na matumaini kwamba viongozi hao wastaafu wangesaidia
kumaliza tatizo hilo. Hata hivyo, Membe alikuwa amewaeleza waandishi wa
habari kuwa, Ziwa Nyasa ni urithi wa nchi tatu za Tanzania, Malawi na
Msumbiji na kwamba siyo sahihi kwa upande wowote kati ya nchi hizo kudai
unamiliki sehemu kubwa ya ziwa hilo.
Tumetiwa moyo na kauli ya Rais Kikwete kwamba
mgogoro huo bado unazungumzika na kwamba nchi hizo mbili bado zinao
uwezo wa kumaliza tatizo hilo pasipo kuhitaji wasuluhishi kutoka nje.
Hata hivyo, tungependa kutoa angalizo kwa Serikali yetu kwamba mgogoro
huo wa mpaka kati yetu na Malawi sasa umeingia katika hatua nyeti na
muhimu, hivyo kauli zote zinazohusu mgogoro huo lazima zitolewe kwa
tahadhari kubwa ili kuepuka kuupa upande wa pili kisingizio cha kujitoa
katika usuluhishi huo.
Kama tulivyoshuhudia mwenendo wa mgogoro huo huko
nyuma, baadhi ya kauli za viongozi wetu hakika zilionekana kuchochea
kuvunjika kwa mazungumzo hayo kwa sababu upande wa pili ulihisi Tanzania
haikuwa na dhamira ya kupata mwafaka wa mgogoro huo.
Tunachotaka kusema hapa ni kuwa, pamoja na ukweli
kwamba Serikali ina kila sababu za kupinga hatua ya Malawi kudai kwamba
eneo lote la Ziwa Nyasa liko katika himaya yake, Serikali yetu hiyo
iache kutumia vyombo vya habari kuelekeza lawama upande wa pili. Kama
alivyosema Rais Kikwete, Serikali lazima ithamini vikao vya usuluhishi.
Pamoja na kauli hiyo ya Rais, tungependa kushauri
kwamba Serikali itafanya vyema kwa kutambua kuwa, huu sasa ni wakati wa
kutumia mbinu za kidiplomasia kuzishawishi nchi marafiki na jumuiya ya
kimataifa kwa jumla kwamba mpaka kati ya nchi hizo mbili uko katikati ya
ziwa hilo. Tunasema hivyo kwa kuwa, Tanzania iko katika nafasi nzuri ya
kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa katika mgogoro huo, kutokana na
ukweli kwamba tangu uhuru imekuwa na sera ambazo siyo tu zimeifanya iwe
kisima cha amani na kimbilio la wanyonge duniani kote, bali pia imekuwa
moja ya nchi chache zinazoendelea ambayo imekoga nyoyo za jumuiya ya
kimataifa kama mfano wa kuigwa.
Tunapendekeza pia kuwa, Serikali ibuni mkakati wa
kidiplomasia kwa kuwatumia mabalozi wake na wasomi waliobobea kupeleka
hoja zake kwa nchi na jumuiya mbalimbali zenye ushawishi, lengo likiwa
ni kutaka msimamo wetu uiridhishe dunia kwamba hakika mpaka wetu na
Malawi uko katikati ya ziwa hilo.
Sisi tunadhani kwamba Serikali haijachelewa
kufanya hivyo. Jambo muhimu ni kwa viongozi wetu kutambua kuwa, katika
wakati tuliomo mchakato wa usuluhishi na upatanishi wa migogoro una
taratibu zake na kwamba siasa za diplomasia ya kimataifa haziendeshwi
kwa fujo, kelele wala ubabe, bali kwa ushawishi na mashauriano miongoni
mwa pande zote husika.
Ni matumaini yetu kwamba kupatikana kwa mafuta na
gesi katika ziwa hilo hakutazifanya nchi zetu hizi majirani kutangaza
uadui. Kauli ya Rais sasa inatupa matumaini mapya kwamba mgogoro huu
utamalizika kwa njia ya maridhiano.
No comments:
Post a Comment