IDADI ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na ujambazi katika matukio mawili tofauti kwenye Parokia za Kanisa Katoliki za Kihsesa na Isimani mkoani Iringa imeongezeka na kufikia nane huku mmoja wa watu waliokamatwa akiwa ni Dereva wa Paroko wa Parokia ya Isimani, Padri Angelo Burgio.
Tukio hilo ambalo lilisababisha mapadri wawili wa
Parokia ya Isimani ambao ni Paroko wa Kanisa hilo Padri Burgio na
msaidizi wake Padri Herman Myala na mlinzi wa Parokia ya Kihesa,
Batholomeo Nzigilwa kujeruhiwa na kulazwa katika hosptali ya Rufaa ya
Mkoa wa Iringa lilitokea usiku wa Novemba 15 na 16 mwaka huu.
Akitaja orodha hiyo mpya huku akisisitiza kuwa
msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine unaendelea Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Iringa, Michael Kamuhanda alisema miongoni mwa watuhumiwa
waliokamatwa ni pamoja na Dereva wa Paroko huyo ambaye hivi karibuni
ndiye aliyemsindikiza kwenda kuchukua fedha Benki.
“Idadi ya watuhumiwa hadi sasa imefikia 8 na kati
ya watuhumiwa wanne waliokamtwa jana katika msako unaoendelea hivi sasa
mmoja wao ni Dereva Baba Paroko na ndiye aliyempeleka hivi karibuni
kwenda Iringa Mjini kuchukua fedha,” alisema Kamuhanda.
Wakati hayo yakiendelea, Serikali imesema vitendo
vya uvamizi wa Parokia za Kanisa Katoliki za mkoani Iringa hauna uhusino
na migogoro yoyote ya kidini inayoendelea nchini bali wahusika
walifanya tendo hilo kwa tamaa ya kujitatia utajiri wa haraka.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mapadri
waliojeruhiwa kwa kwa risasi na mapanga wa Parokia ya Isimani mkoani
Iringa Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu
wa Mbunge William Lukuvi alisema Serikali imejipanga kukomesha vitendo
hivyo vya uhalifu hasa vinavyofanyika katika maeneo wanakoishi mapadri
wakigeni.
“Serikali itahakikisha inaimarisha ulinzi hususani
katika maeneo wanakoshi wamisionari kutokana na watu kujenga dhana kuwa
kila anapoishi mzungu huenda kuna fedha ama mali wanazoweza kujipatia
kwa nguvu kama walivyowafanyia mapadre wa Isimani,” alisema Lukuvi.
Pia wazili Lukuvi alilitaka Jeshi la Polisi mkoani
hapa kutoa mafunzo maalumu kwa watu wanaofanya kazi za ulinzi kwenye
nyumba zote za misheni wanazoishi mapadri wawe na mbinu za kuwabaini kwa
haraka majambazi na kuwadhibiti kabla ya kusababisha madhara.
"Hawa walinzi ambao wanalinda maeneo mbalimbali
katika misheni, taasisi na maeneo mengine wanatakiwa wapewe mafunzo ya
ulinzi ili amani iwe ya kuaminika katika maeneo hayo… jeshi la polisi
kwa sasa wajipange ili watoe mafunzo hayo kwa mfumo huo tunaweza kuzuia
matukio ya wizi na watu kuvamiwa," alisema Lukuvi.
Naye Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hosptali hiyo,
Dk Faustine Gwanchele alisema afya ya mapadri hao akiwemo Paroko Burgio
aliyefanyiwa upasuaji na kutolewa risasi tano mwilini inaendelea vizuri.
“Kwa sasa hali ya Padri Burgio inaendelea vizuri
baada ya kumfanyia upasuaji na kutoa risasi tano mwilini mwake, pia hali
ya Padri Hermani aliyecharangwa kwa mapanga inaendela vizuri isipokuwa
mlinzi aliyepigwa kichwani katika Parokia ya Kihesa, Botholomeo Nzigilwa
hali yake ni mbaya na tumempatia rufaa ya kwenda Muhimbili,” alisema Dk
Gwanchele.
Akizungumzia tukio hilo akiwa hospitalini
alipolazwa Padri Myala (36) ambaye ni msaidizi wa Paroko wa Parokio hiyo
alisema majambazi walikuwa na mwenyeji kwani walionyesha wanajua kila
kona ya majengo ya Parokia hiyo.
No comments:
Post a Comment