Sunday, November 18, 2012

Kigogo wa Polisi ahusishwa na mihadarati


 
Kwa ufupi
“Tukikamata hao vijana wanapiga simu kwa bosi wakishamweleza anawaambia nipe niongee nao anakukaripia ile mbaya sisi tumeacha kabisa hatukamati mirungi, ”alidokeza mmoja wa polisi.


KIGOGO mmoja wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Kilimanjaro anatuhumiwa kuwakingia kifua wafanyabiashara wanaoingiza Mirungi kutoka nchini Kenya.
Mwananchi lilidokezwa kuwa kushamiri kwa uingizaji mirungi nchini kupitia Wilaya ya Moshi Vijijini na Mwanga kuna uhusiano wa moja kwa moja na kigogo huyo wa polisi anayewakingia kifua.
Inadaiwa kuwa kuhusishwa kwa kigogi huyo kunatokana na wafanyabiashara hao kuwa na kiburi kupindukia na kila wanapokamatwa humpigia simu ofisa huyo na kuwashitaki polisi wanaowakamata.
“Tukikamata hao vijana wanapiga simu kwa bosi wakishamweleza anawaambia nipe niongee nao anakukaripia ile mbaya sisi tumeacha kabisa hatukamati mirungi, ”alidokeza mmoja wa polisi.
Polisi huyo aliongeza kuwa “We unajua jeshi letu lilivyo hivi sasa utajikuta unahamishiwa pembezoni huko hata ukiiona Sh2,000 unashukuru Mungu…nani anayataka hayo?”alihoji.
Bidhaa hiyo ambayo imekuwa na soko kubwa katika miji ya Arusha,Mererani,Moshi na miji jirani husafirishwa kwa pikipiki kutoka Kenya na wastani wa pikipiki nane huvuka mpaka kila siku.
“Wanaifunga kwenye maboksi makubwa na kila boksi linaweza kuwa na mirungi ya kama Sh1,500,000 hadi Sh2,000,000 kutegemeana na ukubwa na sasa hivi hii ndio deal (biashara),”alidokeza raia mmoja(Jina linahifadhiwa).
Kwa mujibu wa chanzo cha habari alieleza kuwa mirungi hiyo huingizwa ikitokea kwa Robert Kenya kupitia eneo la Relini Makuyuni na kutokea Kileo na kisha kushika barabara ya Kahe na kutokea Mabogini Wilaya ya Moshi Vijijini.
Njia nyingine inayotumiwa na wafanyabiashara hao ni ile ya Kitobo au Maria Tabu nchini Kenya hadi vijiji vya Saghana na Makuyuni na kisha kuingia katika mji mdogo wa Himo.
Baada ya mirungi hiyo kufikishwa Mabogini, Himo na Njiapanda, hupakiwa kwenye magari binafsi, mabasi ya abiria na wakati mwingine kwa pikipiki hadi Moshi, Mererani na Arusha.
Wakati mwingine wafanyabiashara hao hutumia barabara ya kuanzia Kitobo-Mnoa-Kileo na kupakia kwenye mabasi alfajiri kila siku kwenda Moshi mjini, Mererani na Arusha.
Pia ipo Mirungi mingine inayosambazwa kutokea Makanya na Hedaru na kudaiwa kuwa hulimwa maeneo ya milimani katika kata ya Vudee na kitongoji cha Saweni wilayani Same.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...