Akizungumza katika mkutano maalumu wa maombi ya kuombea taifa yaliyofanyika mjini Moshi na kuhudhuriwa na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Askofu Gadi alisema kuporomoka kwa kasi kwa maadili miongoni mwa Watanzania wakiwamo baadhi ya viongozi, kumesababisha usimamizi mbovu wa rasilimali.
Alizitaja rasilimali hizo kuwa ni pamoja na madini, vivutio vya utalii, Mlima Kilimanjaro na kadhalika.
Alisema nchi zilizoendelea na ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi kunatokana na kujenga maadili mema na kumcha Mungu kwa vitendo. Akitolea mfano wa kupungua kwa kasi kwa theluji katika Mlima Kilimajaro, Askofu Gadi alisema hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira kando kando ya mlima huo ambao chanzo chake ni kuporomoka kwa maadili na kukosa ufunuo wa Mungu.
“Tukiweza kujenga maadili mema katika vizazi vyetu
hakutakuwa na uzinzi, rushwa, uonevu, ubinafsi na uharibifu wa
mazingira unaotishia kutoweka kwa theluji katika mlima wetu maarufu
barani Afrika wa Kilimanjaro,” alisema.
Kadhalika Askofu huyo aliwaasa Watanzania kulinda
amani na umoja wa taifa kwa nguvu zao zote na kamwe wasikubali
kurubuniwa au kutenganishwa na watu wachache au kundi la watu kwa imani
za kidini au itikadi za kisiasa.
Alisema watu wanapaswa kufahamu kuwa amani ikitoweka, kuirejesha ni vigumu na ni gharama kubwa.
No comments:
Post a Comment