Wednesday, November 14, 2012

AJALI YATOKEA DARESALAAM, BASI LA UDA YAUWA WATU WAWILI


Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Temeke, Prackson Rugazia (katikati) akizungumza na waandishi jana kuhusu ajali ya basi la Uda na roli iliyotokea eneo la Mbagala Mission na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhiwa 47.  Picha na Venance Nestory 

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 47 kujeruhiwa baada ya gari la Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), linalofanya safari zake kutoka Mbagala kwenda Gongo la Mboto kupata ajali eneo la Kiwanda cha Nguo cha KTM Mbagala.
Ajali hiyo ilitokea jana  saa 7:30 asubuhi barabara ya Kilwa, eneo la Kiwanda cha Nguo cha Mbagala, basi la  Shirika la usafiri Dar es Salaam (Uda) likiwa limebeba zaidi ya abiria 50 kuchomekewa na gari ndogo kwa mbele na kusababisha ajali hiyo.
Akizungumza Dar e salaam jana, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Temeke, Prackson Rugazia alisema majeruhi walipelekwa  Hospitali ya Temeke kwa matibabu zaidi.
Rugazia alisema tukio hilo lilitokea baada ya gari ndogo lililokuwa likitokea barabara za mitaani kukatisha ghafla na kusababisha dereva wa Uda kushindwa kujizuia na kuingia kwenye mtaro.
“Ni kweli watu wawili wamefariki na wengine 47 wamejeruhiwa baada ya kutokea kwa ajali iliyohusisha gari la abiria la Shirika la Usafiri la Dar es Saalaam (Uda),  kuingia kwenye mtaro baada ya kukatisha ghafla gari ndogo iliyokuwa ikitokea barabara za mtaani,” alisema Rugazia.
Aliongeza kuwa baada ya kutokea ajali hiyo, wananchi walijitokeza na kuwasaidia abiria waliokuwa kwenye Uda, wengine waliondoka kutokana na kupata majeraha kidogo.
Alisema kutokana na hali hiyo, maiti za watu hao zimehifadhiwa Hospitali ya Temeke huku majeruhi wanne wakiwa na hali mbaya na kwamba, wanaendelea na matibabu.
Rugazia aliwataja waliokufa kuwa, ni Baraka Amani (16) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu Sekondari ya Chanika na mmoja jina lake halijajulikana.
Alisema mwili wa mtu huyo haukuweza kutambulika kutokana na kutokuwa na kitambulisho chochote.
Aliwataja  majeruhi ambao hali zao ni mbaya kuwa, ni Andrew Simon (30), Rashid  Sultan, Mary William (48) na Watende Saidi (37) ambaye alitarajiwa kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...