MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) amesema yupo tayari kuipa Serikali wachunguzi wa kimataifa iwatumie kuchunguza Watanzania walioficha fedha haramu kwenye Benki za Uswisi.
Kauli hiyo ya Zitto imekuja takriban wiki moja tangu alipoieleza Serikali kwamba kama imeshindwa kuwachunguza walioficha fedha Uswisi, iwaachie wenye uwezo wa kufanya suala hilo yenyewe isubiri majibu kwa manufaa ya nchi.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, alisema kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika kuwataka Watanzania kupeleka majina ya vigogo walioficha mabilioni kwenye benki hizo ili wachunguzwe, inaingilia uhuru wa Bunge na kwamba alitakiwa kuzungumza jambo hilo bungeni.
Pia, alisema lingekuwa jambo la busara kama Spika wa Bunge, angeweka wazi ripoti ya kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza tuhuma za wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa, ili umma uweze kufahamu kwa undani juu ya uchunguzi huo.
Akizungumza na Mwananchi Dar es Salaam jana, Zitto alisema kutaja majina ya Watanzania hao siyo suluhisho, kinachotakiwa ni nchi kuwa na utaratibu mzuri wa kubaini fedha zinazofichwa nje na kusisitiza kuwa siyo lazima iwe Uswisi. Alisema Desemba 10, mwaka huu anatarajia kwenda Uswisi kukutana na watafiti wake, huku mmoja akiwa anatokea Uingereza na kwamba, atawapatia taarifa ya mahali taifa lilipofikia kuhusiana na fedha hizo.
“Ni muhimu kuacha uchunguzi ukafanyika ili kuwabaini waliohusika kuliko kutaja majina ya watu. Ninaweza kutaja majina watu wakasema natafuta umaarufu,” alisema Zitto na kuongeza:
“Nikionana na watafiti hawa nitawaomba kama watakuwa tayari kutoa ushirikiano na timu ya uchunguzi inayofuatilia suala hilo, moja ya jambo ambalo nitawaomba ni kutoa ushirikiano wao kwa taifa kama watakuwa tayari ili watusaidie kubaini majina hayo ambayo siyo yapo Uswisi peke yake bali na nchi nyingine.”
Alisema Watanzania waache kupenda mambo rahisi na kwamba, uchunguzi lazima ufanyike kuwabaini walioficha mabilioni hayo ili fedha hizo zirejeshwe nchini.Alisema Serikali ya Uswisi haiwezi kuisaidia Tanzania kufanya uchunguzi wa fedha hizo.
No comments:
Post a Comment