MKUU wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila ameshukuru Serikali ya Japan kwa jitihada za kusaidia mkoa huo katika utekelezaji wa maendeleo.
Mwananzila alitoa shukrani hizo kwenye utiaji saini wa dola 120,762 za Marekani, kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa mabweni mawili ya Sekondari ya Kata ya Ng’apa, Manispaa ya Lindi.
Akizungumza baada ya zoezi hilo la utiaji saini, Mwananzila alisema Japani imekuwa ikiwasaidia kwa sekta elimu, itakayowezesha vijana wa mkoa huo kujiandaa kwa maisha ya baadaye.
Mwananzila amesema Lindi inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwamo uchache wa sekondari za kidato cha tano na sita na mabweni.
Alisema mkoa unahitaji mabweni 334, yaliyopo hivi sasa ni 64 na kufanya kuwapo kwa upungufu wa mabweni 280.Alisema kuna Sekondari 120 zikiwamo 115 za serikali na tano za watu binafsi, nne ndizo zenye kidato cha tano na sita.
Alizitaka halmashauri kuwa karibu wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo, ili kuwa na ufanisi usio na matatizo.Pia, aliomba Taasisi ya Women Social Entrepreneurship kuendelea kutafuta fursa zingine za maendeleo kwa ajili ya wananchi wa Tanzania.
Naye Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada alisema Japan imeamua kutoa msaada huo kwa lengo la kuboresha elimu, hususan kwa wanafunzi wakike.
Okada alisema elimu kwa wasichana ni muhimu kwani itatoa fursa kwao kushiriki katika ujenzi wa taifa.
“Niliposikia mkoa unahitaji kuboresha elimu ya wanafunzi wasichana, nikasema hii ni habari njema kwa taifa linalolenga kuleta maendeleo zaidi…
kwani elimu kwa wanawake ni muhimu sana itakayotoa fursa ya kushiriki katika sekta za ujenzi wa taifa lao,” alisema Okada.
No comments:
Post a Comment