Saturday, November 17, 2012
UWANJA WA NDEGE MBEYA WAVAMIWA NA WAGENI KUTOKA NJE.
UWANJA wa ndege wa kimataifa Jijini Mbeya ulio katika hatua za mwisho za ujenzi unadaiwa kuvamiwa na watu kutoka nje ya mkoa kwa lengo la kuwekeza vitega uchumi.
Wavamizi hao wanadaiwa kutoka katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha,Morogoro na nchi jirani Zambia,Kenya na Malawi ambao inasemekana kuwa wameanza kujitwalia maeneo yaliyo jirani na uwanja kwa ajili ya vitega uchumi baada ya kusikia kuwa Serikali ipo mbioni kufungua uwanja huo.
Katibu wa Madiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Mkoa wa Mbeya, Geofrey Kajigili alibainisha tukio hilo kwa waandishi wa habari jijini Hapa.
“Nina uhakika na ninachokisema kwenu na kwamba nina ushahidi wa watu kutoka Moshi, Arusha na baadhi ya nchi jirani kama Kenya, Malawi na Zambia ambao wamejitwalia maeneo kwa kuyanunua kutoka kwa wananchi wa eneo hilo kwa ajili ya kuweka vitega uchumi,” alisema Kajigili.
Kufuatia kuwapo kwa hali hiyo Kajigili aliwataka wakazi wa mkoa wa Mbeya kuwa makini na ardhi yao na wasikubali kuiuza ovyo badala yake ndio wajipatie fursa ya kujiwekea vitega uchumi katika maeneo hayo.
Aidha, alisema kuwa wakazai hao wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo ya kufunguliwa kwa uwanja huo wa ndege wa kimataifa kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi badala ya kuwa watazamaji wa wageni walioanza kuingia kinyemela katika maeneo hayo.
Mbali na hilo, Kajigili alisema kuwa Serikali Mkoani hapo inawajibu wa kuwahamasisha wananchi wake kuwekeza kwenye maeneo hayo kwa kuwa ni fursa muhimu ya uchumi kwa wakazi hao na sio kuwaachia wageni wanufaike peke yao.
Kwa mujibu wa Kajigili, Serikali inatakiwa kuwa na mipango ya muda mrefu kwa kuandaa ardhi ya kutosha wakati huu kwa ajili ya matumizi ya baadaye badala ya kusubiri wananchi wawekeze na kisha kuwabomolea nyumba zao pale Serikari inapotaka kutumia ardhi hiyo kwa shughuli nyingine za kimaendeleo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment