Saturday, November 24, 2012

SHEHENA YA DAWA ZA MALARIA YAIBWA, JE NANI ANAHUSIKA? BOFYA HAPA





DOZI 35,000 kati ya 78,000 za dawa ya kutibu malaria aina ya Artequick, zilizotolewa kama msaada kwa Tanzania na Serikali ya China, zimepotea katika mazingira ya kutatanisha, Mwananchi imebaini.
Imebainika kuwa dawa hizo zilizokuwa zigawiwe bure kwa wagonjwa katika hospitali za Serikali nchini, sasa zinauzwa kwa kati ya Sh9,000 hadi Sh12,000 kwenye maduka na hospitali binafsi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na vyanzo vya kuaminika zinabainisha kuwa, dawa hizo zimeibwa, au zikisafirishwa kwenda Zanzibar au baada ya kufikishwa huko na sasa zinauzwa mitaani.
"Dawa zilipofika dozi hizo 35,000 ilionekana zipelekwe Zanzibar kwanza halafu zinazofuata zisambazwe mikoa ya Tanzania Bara, lakini cha ajabu hivi sasa dawa hizo zinauzwa katika maduka ya jumla ya dawa na ya rejareja," kimeeleza chanzo hicho.
Chanzo hicho kinabainisha kuwa, paketi za dawa hizo zilikuwa zimeandikwa pembeni 'Not for Sale’ (siyo kwa ajili ya kuuzwa) ambayo yamefutwa kwa kupakwa rangi nyekundu ili yasionekane.
Mkurugenzi wa Tiba katika Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), akizungumza kupitia kwa Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo, Gaudencia Simwanza alikiri kukamatwa kwa dawa hizo za msaada kutoka China ambazo zilikuwa zinauzwa mitaani na kueleza kuwa, wapo katika uchunguzi.
Ni kweli tumekamata dawa hizo za msaada zilizotolewa na China kwa ajili ya hospitali za Serikali nchini na zilizoibwa ni zile zilizotakiwa kusambazwa Zanzibar," alisema Simwanza na kuongeza kuwa, ni mapema mno kueleza kiasi cha dawa kilichokamatwa.
Simwanza aliongeza kuwa, kimsingi dawa hizo zimekutwa katika eneo ambalo hazitakiwi kuwepo na kwamba hilo ni kosa kisheria na hali hiyo inaashiria kufanyika kwa wizi.
“Kukutwa na mali ya wizi ni kosa kisheria, kwahiyo tunafanya uchunguzi zaidi ili kubaini kiasi cha wizi ambao umefanyika,”alisema Simwanza.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani alikiri kupokea dawa hizo za msaada kutoka China na kwamba, boksi zote 88 zilizopokewa zipo salama.
“Ni kweli tumepokea dawa hizo boksi 88 sawa na paketi 35,000 lakini dawa zote zipo salama na hatujaanza kuzisambaza,” alisema Mwaifwani na kuongeza kuwa msaada huo ulipokewa Novemba 6 mwaka huu.
Alisema hajui hizo ambazo zinauzwa zikiwa zimefutwa maandishi zimetoka wapi na kusisitiza kuwa walizonazo zina maandishi ya ‘Not for Sale’ pembeni ya paketi.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...