WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amesema kuna mkono wa vigogo katika biashara haramu ya pembe za ndovu na kuahidi kuwa atapambana nao hadi mwisho.
Kauli hiyo ya Kagasheki inakuja siku chache baada ya shehena kubwa ya pembe za ndovu kukamatwa na maofisa usalama nchini Hong Kong ikitokea Tanzania.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
dada la Mwananchi la The Citizen, Balozi Kagasheki alithibitisha kuwa
pembe hizo zenye thamani ya Sh2.4 bilioni zilitokea nchini na kusema
inaonekana kuna mkono wa watu wazito katika biashara hiyo.
Aliwashukia maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuwa hawakuchukua hatua
stahili katika kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu na
kuongeza kuwa ni jambo lisiloingia akilini mzigo mkubwa kama huo upakiwe
nchini bila mamlaka husika kujua.
“Napenda sasa kutangaza vita na wale wote
wanaohusika katika biashara hii haramu, nitapambana nao. Hali hii
inanifanya niamini kuwa kuna mkono wa vigogo katika mtandao huu,”
alisema Kagasheki na kuongeza:
“Uchunguzi wetu hautamwacha mtu hata mmoja na hatua za kisheria zitachukuliwa.”
Aliongeza kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, atafanya mabadiliko makubwa katika Idara ya Wanyamapori, mapori ya akiba na hifadhi za taifa.
Aliongeza kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, atafanya mabadiliko makubwa katika Idara ya Wanyamapori, mapori ya akiba na hifadhi za taifa.
Kwa mujibu wa Waziri Kagasheki, ameshawasiliana na
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema na wamekubaliana kuunda
timu itakayofanya uchunguzi wa suala hilo.
Kuhusu pembe hizo zilizokamatwa, Kagasheki alisema alipata taarifa kutoka Dubai zilizothibitisha kuwa shehena hiyo ilitoka Tanzania na hati za mzigo huo zilionyesha kuwa makontena hayo yalikuwa yamebeba alizeti kutoka Tanzania kwenda Dubai.
Kuhusu pembe hizo zilizokamatwa, Kagasheki alisema alipata taarifa kutoka Dubai zilizothibitisha kuwa shehena hiyo ilitoka Tanzania na hati za mzigo huo zilionyesha kuwa makontena hayo yalikuwa yamebeba alizeti kutoka Tanzania kwenda Dubai.
Alisema kuwa pembe 569 zilikamatwa kutoka katika makontena hayo na hivyo, ikamaanisha kuwa zaidi ya ndovu 150 waliuawa nchini.
Maofisa wa Forodha wa Hong Kong walikamata zaidi
ya tani moja ya pembe za ndovu zenye thamani ya Dola za Marekani 1.37
milioni katika soko la pembe za ndovu nchini China.
“Pembe hizo zilikuwa zimefichwa pamoja na bidhaa
nyingine. Kulikuwa na magunia 400 ya mbegu za alizeti zilizotumika
kuficha ukweli,” alisema Mkuu wa Komandi Baharini na Bandari wa Hong
Kong, Wong Sui-hang.
Alisema pembe hizo zilisafirishwa kutoka Tanzania
kwa meli kabla ya kupakiwa kwenye meli nyingine zilipofikishwa Dubai na
kuanza kusafirishwa kwenda Hong Kong.
Oktoba mwaka huu, maofisa usalama nchini China
walikamata karibu tani nne za pembe za ndovu zenye thamani ya Dola 3.4
milioni zilizosafirishwa kutoka Tanzania na Kenya.
Baada ya shehena hiyo kukamatwa, gazeti dada la
The Citizen liliripoti kuwa uchunguzi uliofanywa na Shirika la Polisi la
Kimataifa (Interpol) ulibaini kuwa kuna Watanzania wanne waliohusika
katika usafirishaji wa pembe hizo.
No comments:
Post a Comment