SHIRIKA la Vijana la Tanzania youth Alliance (Tayoa), limewataka vijana nchini kuwa na moyo wa uzalendo, kuipenda nchi yao na kulinda rasililimali za nchi, ili ziwe na manufaa kwa vizazi vijavyo. Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa shirika hilo, Peter Masika, baada yakupewa tuzo ya heshima kwa mchango wake katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Tuzo hiyo iitwayo Gail Goodridge, imetolewa
na Shirika la AfricomNet la mjini Nairobi Kenya na Masika amekuwa mtu
wa kwanza kupewa tuzo hiyo tangu ilipoanzishwa, mapema mwaka
huu.
Masika alisema tuzo hiyo imempa ari mpya katika kupambana na
maradhi ya Ukimwi na kuhamasisha vijana kujilinda dhidi ya
maambukizi.
“Kutambuliwa katika bara zima la Afrika hasa kwa Tayoa
kutumia Teknohama katika kupambana na Ukimwi, ni heshima kubwa sana,
mimi nawaomba vijana wasikate tamaa na waipende nchi yao kama ambavyo
tunaona vijana wa nchi mbalimbali wakizipenda nchi zao,” alisema.
Alisema yeye binafsi amejitolea kutumia
muda wa maisha yake, kuelimisha vijana kuhusu ugonjwa wa Ukimwi na ndiyo
sababu ya kutambuliwa kwake.
Alisema viongozi wenye dhamana nao
wanapaswa kuweka mbele uzalendo na utaifa kwa kutunza rasilimali za nchi
kwa maslahi ya wananchi wote, ili vijana waige kutoka
kwao.
Aliwashauri vijana kufuatilia masuala ya demokrasia na utawala
bora, ili wajue masuala mbalimbali yanayohusu nchi yao na wajitolee
kufanyakazi, ili wapate ujuzi.Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Kupambana na Ukimwi (Tacaids), Dk. Fatma Mrisho, aliipongeza Tayoa kwa kupata tuzo hiyo na kuishauri iendelee na jitihada za kupambana na Ukimwi. Alisema elimu kuhusu Ukimwi, inahitajika kwa kiwango kikubwa hivyo kuwepo kwa mashirika yanayotoa elimu hiyo ni faraja kubwa kwa serikali. Mwisho
No comments:
Post a Comment