WATU wanne ambao ni wafanyabiashara wa ng’ombe
wanashikiliwa na polisi mkoani Manyara wakidaiwa kukutwa na noti bandia
zenye thamani ya zaidi ya Sh3 milioni walizokuwa wanazinunulia mifugo
hiyo mkoani humo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Manyara,
Kamishna Msaidizi Akili Mpwapwa,tukio hilo lilitokea juzi wilayani
Hanang’ kwenye mnada wa kununulia ng’ombe ambapo watu hao walikamatwa
wakati wakinunua mifugo hiyo.
Kamanda Mpwapwa aliwataja watu hao kuwa wote ni wakazi wa wilayani Mbulu mkoani Manyara.
Alisema watu hao ambao ni wafanyabiashara wa
mifugo walikuwa wananunua ng’ombe wanne kwa wafanyabiashara watatu ambao
ni Detugwa Makotw (43),Jumanne Sesha (75) na John Gemahi (52).
Alisema watu hao walinunua ng’ombe wanne kwa
wafugaji hao na kutoa noti za bandia kiasi cha Sh1.9 milioni zilizokuwa
kwenye noti za Sh10,000 ambapo walikutwa pia na noti nyingine za bandia
sawa na Sh1.7 milioni.
“Watu hao walikamatwa kutokana na ushirikiano wa
polisi na raia wema kwani ilibainika kukithiri kwa tabia hiyo hasa
wakati wa kununua mifugo kwenye minada mkoani humo,” alisema Kamanda
Mpwapwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa upelelezi na makosa ya
jinai mkoani Manyara, Benedict Msuya alisema wamefanikisha kukamata
wafanyabiashara hao ambao walikithiri na tabia hiyo ya kununua mifugo
kwa kutumia noti bandia.
Msuya alitoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kuwa na
tahadhari pindi wanapokuwa wauza au kununua mifugo au bidhaa nyingine za
thamani kwa kuchunguza noti hizo za bandia.
No comments:
Post a Comment