Thursday, November 15, 2012

Tume ya sayansi yajiandaa kuwanufaisha wakulima

TUME ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imeandaa mpango maalumu kwa ajili ya kuanza kuwasaidia wakulima nchini ili waweze kunufaika kupitia kilimo.Mpango huo unatarajiwa kuanza mwakani na utawahusisha wakulima wote nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Uhawilishaji na Uendelezaji Sayansi na Teknolojia wa Costech, Dk Dugushilu Mafunda alisema wakulima wengi wamekuwa wakilima kwa mazoea huku wakiwa hawana ushauri wa ufundi.
“Huu ni mpango maalumu wa agro business… tunayalea mawazo yao hadi wanaingia kwenye soko kwa sababu wengine hawana hata ushauri wa ufundi au elimu ya biashara,” alisema Dk Mafunda.
Pia, Costech imewashauri watu wenye ugunduzi mbalimbali ambao hawana uwezo wajitokeze kusaidiwa ili uweze kuendelezwa.
Kwa muda mrefu sasa tume hiyo imekuwa ikiwasaidia wagunduzi na wajasiriamali kuwapatia mafunzo, ushauri wa kitaalamu na fedha ili kufanikisha mawazo yao.
Mkurugenzi huyo alisema lengo lao ni kuwatambua wagunduzi walionao ili kuwajengea uwezo na kufanikisha ugunduzi wao kufika sokoni.
“Watu wenye mawazo ya ugunduzi wajitokeze wasaidiwe, kwa sababu tunatoa msaada kwa wajasiriamali na watu wote wanaojihusisha na uendelezaji uhawilishaji wa sayansi na teknolojia,” alisema.
Alisema katika mpango huo, mgunduzi hutakiwa kupeleka mchanganuo kuhusiana na kile anachotaka kukifanya, baada ya Costech kujiridhisha humwezesha mgunduzi huyo.
Alisema mgunduzi husika hujengewa uwezo wa kuingia kwenye soko na kupata faida na kwamba, akishindwa hawezi kupewa tena fedha badala yake hutakiwa kurejesha alizopewa.
Miongoni mwa walinufaika kupitia mpango huo, ni Shirika la Kutengeneza Magari la Nyumbu ambalo hivi karibuni lilipatiwa Sh200 milioni kwa ajili ya kutengeneza vipuri mbalimbali vya garimoshi zikiwamo breki.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...