WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema wakati umefika kwa sasa hapa nchini elimu ya Sekondari iwe elimu bure na kumwondolea mwananchi wa kawaida mzigo wa kubeba gharama za elimu hiyo.
Lowassa akizungumza jana mjini Babati alisema,
mjadala kuhusu elimu kutolewa bure hadi sekondari haukwepeki, hivyo
kuwataka wadau wa elimu kuanza sasa kujadili suala hilo na kwamba Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa kulifanya hilo kuwa moja ya ajenda zake
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alisema elimu ya sekondari ikifanywa bure, itakuwa
ni fursa kwa kila mtoto wa Kitanzania kuipata. Hatua ambayo itaongeza
weledi na uelewa wa mambo mengi katika jamii.
“Ninasema sasa wakati umefika elimu ya sekondari
kuwa kama elimu ya msingi kwa watoto kusoma bure kuanzia kidato cha
kwanza hadi kidato cha nne,” alisisitiza Lowassa ambaye ni Mbunge wa
Monduli (CCM).
Kwa kauli hiyo, Lowassa ni kama ameunga mkono Sera
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao waliingia katika
mgogoro na CCM kuhusu elimu kutolewa bure wakati wa kampeni za Uchaguzi
Mkuu wa 2010.
Chadema wamekuwa wakisisitiza kwamba elimu bure
inawezekana hadi ngazi ya sekondari, lakini wakati wote CCM wamekuwa
wakisema kuwa suala hilo haliwezekani na kwamba kauli za aina hiyo ni
kuwahadaa wananchi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, aliyekuwa mgombea wa
urais kupitia Chadema, Dk Willibrod Slaa alitumia sera ya elimu bure
kuanzia chekechea hadi sekondari kama kete ya kusaka ushindi, huku
akisema chama chake kingetenga asilimia 35 ya bajeti kwa ajili ya
kuboresha elimu na kutoa elimu bure.
Hata hivyo, aliyekuwa mgombea wa CCM na baadaye
kupata ushindi, Rais Rais Jakaya Kikwete alikuwa akiwatahadharisha
wapigakura kuwa kwamba ahadi ya Chadema ni hewa na kwamba hilo
lisingewezekana.
Mvutano huo uliwaingiza makada wengine ambao ni
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye wakati huo alikuwa Meneja
Kampeni wa CCM na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel
Sitta na kwa upande wa Chadema, Dk Kitila Mkumbo naye alijitokeza
kutetea sera ya chama chake.
Katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika
Novemba 10, 2010 katika Kata ya Mchangimbore katika Jimbo la Peramiho
mkoani Ruvuma, Rais Kikwete alisema “Serikali haiwezi kutoa huduma za
jamii bure” na kwamba lazima wananchi wachangie.
“Nimebahatika kukaa serikalini muda mrefu hiyo
sera ya bure tulijaribu na ikatushinda na wakati huo Hayati Baba wa
Taifa, Mwalimu Nyerere, tulikaa naye tukaona hilo haliwezekani tukaamua
tubadilishe sasa nawashangaa wenzetu wanawadanganya eti watatoa bure.”
Kwa upande wake Dk Slaa akiwa mjini Arusha katika
moja ya mikutano yake alisema kwamba CCM walikuwa wakipinga sera ya
elimu bure hadi sekondari kutokana na kulea ubadhirifu na kuthamini
anasa kuliko maendeleo kwa wananchi.
Kauli ya Lowassa
Jana akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati, Lowassa alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kuzungumzia suala hilo bila ya woga.
Kauli ya Lowassa
Jana akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati, Lowassa alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kuzungumzia suala hilo bila ya woga.
No comments:
Post a Comment