Sunday, November 18, 2012

Kikwete kutambulisha safu CCM leo

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete

MWENYEKITI wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kuitambulisha safu yake ya uongozi itakayokiongoza chama hicho katika kutafuta ushindi wa uchaguzi mwaka 2015.
Utambulisho huo utafanywa kwa wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam kwenye utakaofanyika kwenye Viwanya vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Mwenyekiti CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida alisema kuwa, Rais Kikwete ataitambulisha Sekretarieti mpya ambayo ilichaguliwa hivi karibuni mjini Dodoma.
Alisema hii ni fursa ya kipekee kwa wanachama na wakazi wa Dar es Salaam kushuhudia sekretarieti hiyo mpya ambayo imepewa kazi ya kufanya mabadiliko.
Alisema CCM imejipanga upya kwa kuteua sekretarieti hiyo ambayo lengo lake kubwa ni kuleta mabadiliko ambayo yataisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa, tunatekeleza Ilani ya chama chetu kwa vitendo, jambo ambalo limetufanya tujipange upaya ili kuhakikisha kuwa wanachama pamoja na viongozi wanaitangaza sera yetu kwa wananchi,” alisema Madabida.
Aliongeza kutokana na hali hiyo wanaamini kuwa wanaweza kutatua kero mbalimbali zilizojitokeza na zitakazojitokeza ili kuhakikisha kuwa, wanapata ushindi katika chaguzi mbalimbali zijazo iwe za madiwani, hata uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Alisema kutokana na hali hiyo wanaamini kuwa, safu hiyo inaweza kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo bila ya kujali itikadi za vyama vyao, jambo ambalo litaweza kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake.
Mwenyekiti huyo alisema mkakati wao ni kuhakikisha kuwa wanasimamia kaulimbiu yao mpya inayosema; ’Umoja ni Ushindi na Ushindi ni umoja’ jambo ambalo linaweza kuwasaidia kutimiza ahadi walizokusudia.
Safu mpya ya uongozi ndani ya chama hicho iliyochaguliwa katika mkutano huo ni pamoja na Philip Mangula aliyechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti (bara), huku Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti (Zanzibar).
Rais Kikwete pia alimteua kada mkongwe nchini, Abdulhaman Kinana kuwa katibu mkuu.
Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba amechaguliwa kuwa Naobu Katibu Mkuu upande wa Bara na Vuai Ali Vuai upande wa Zanzibar.
Wengine ni Zakhia Meghji aliyeteuliwa kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha, Mohamed Seif Khatib (Oganaizesheni), Dk Rose Migiro (Kimataifa) na Nape Nnauye (Uenezi).
Uteuzi huo ulitanguliwa na uchaguzi ambao ulimrejesha Rais Kikwete kuwa Mwenyekiti wa chama wa Taifa huku kukiwepo na taarifa pamoja na vipeperushi vya kutaka kushinikiza anyang’anywe kofia hiyo ya ndani ya CCM ili abakie na urais.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...