Sunday, November 18, 2012

Kivuli cha Chadema chaitisha CCM

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar  Dk.Ali Mohamed Shein,(katikati) akisalimiana na Wananchi na wanachama wa chama hicho waliofika kumpokea katika  Viwanja vya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar jana,akitokea Dodoma katika Mkutano Mkuu wa Halmashauri ya CCM na Uchaguzi wa Viongozi wa juu katika chama hicho.Picha na Ikulu ya Zanzibar 

KIVULI cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinaonekana kukitisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya jina la chama hicho kutawala katika mkutano mkuu wa CCM uliomalizika Jumanne mjini Dodoma.
Jina la Chadema lilianza kutawala katika mkutano huo, Jumapili Novemba 11 mwaka huu,  wakati makada wa chama hicho waliokuwa wakigombea ujumbe wa Halmashauri Kuu (Nec), wakijinadi kwa wajumbe.
Chadema ilitumiwa na baadhi ya wagombea wa nafasi 10 za Bara na Visiwani kama kete yao ya kuchaguliwa kupata nafasi hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira wakati akiomba kura aliwaambia wajumbe wa mkutano huo wampe kura ili apeleke kilio Chadema.
Alisema akichaguliwa mjumbe wa Nec atapata nguvu ya kupambana na Chadema.
“Nipeni kura ili nipate nafasi nipeleke kilio Chadema,” alisema Wassira huku akishangiliwa wakati akiomba kura na Rais Jakaya Kikwete akimwita kwa jina la utani ‘Tyson’.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho, (UVCCM), Martine Shigela  wakati akiomba kura kwa wajumbe wa mkutano huo alisema yeye ndiye anayeongoza jeshi la ardhini  linalopambana na wapinzani wanaopiga kelele.
“Mimi ndiye ninayeongoza jeshi la ardhini linalopambana na wapinzani wanaopiga kelele,” alisema.
Naye Mwanamanga Manguga aliwaomba wajumbe wampigie kura ili CCM aipeleke Chuo Kikuu cha Dodoma anakosoma na kwamba, tayari ameshaingia katika mapambano.
Alisema katika uchaguzi wa udiwani uliopita Kata ya Msalato mjini Dodoma, wafuasi wa Chadema walimpiga mawe na kumjeruhi wakati akitetea chama hicho.
Chadema pia ilikuwa ikitamkwa sana na mshereheshaji wa mkutano huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Nape Nnauye wakati akitoa matangazo mbalimbali kwa wajumbe. “Watawezaaa… Wataweza hao Chadema…,” alisikika akiwaambia wajumbe wa mkutano huo nao wakimjibu; “Hawaweziii!”
Vilevile, Chadema ilikuwa ikitajwa sana na wapambe wa wagombea wa nafasi ya Nec ambao mara kwa mara walisikika wakiwaambia wachague wagombea wao kwa sababu ndio wenye uwezo wa kupambana na Chadema.
Mpambe mmoja wa mgombea mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake, aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa chama hicho kinapaswa kuchagua safu ya uongozi ambayo itakuwa ni mwiba kwa Chadema.
Hata Rais Jakaya Kikwete wakati akifunga mkutano huo, Novemba 13 mwaka huu, aliwataka wanachama wa chama hicho kuwajibu wapinzani kwa hoja, kama alivyofanya, aliyekuwa Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama hicho, Mwigulu Nchemba wakati wa Bunge la Bajeti mwaka huu.
Alisema, “Baada ya wapinzani kutoa bajeti yao, kijana wetu, Mwigulu alisimama akaivunjavunja bajeti yao. Wakanywea.  Ndivyo tunavyopaswa kufanya.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...