Monday, November 26, 2012

Tz inaweza kuwa kinara wa kiuchumi A. Mshariki

Mwenyekiti wa Shirika la Huduma ya Habari  Njema kwa wote, Askofu Charles Gadi amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwa dola yenye nguvu kubwa kiuchumi katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika, kama  italinda na kuendeleza rasilimali zilizopo.
Akizungumza katika mkutano maalumu wa maombi ya kuombea taifa yaliyofanyika mjini Moshi na kuhudhuriwa na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Askofu Gadi alisema kuporomoka kwa kasi kwa maadili miongoni mwa Watanzania wakiwamo baadhi ya viongozi, kumesababisha usimamizi mbovu wa rasilimali.
Alizitaja rasilimali hizo kuwa ni pamoja na madini, vivutio vya utalii, Mlima Kilimanjaro na kadhalika.
Alisema nchi zilizoendelea na ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi kunatokana na kujenga maadili mema na kumcha Mungu kwa vitendo. Akitolea mfano wa kupungua kwa kasi kwa theluji katika Mlima Kilimajaro, Askofu Gadi alisema hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira kando kando ya mlima huo ambao chanzo chake ni kuporomoka kwa maadili na kukosa ufunuo wa Mungu.
“Tukiweza kujenga maadili mema katika vizazi vyetu hakutakuwa na uzinzi, rushwa, uonevu, ubinafsi na uharibifu wa mazingira unaotishia kutoweka kwa theluji katika mlima wetu maarufu barani Afrika wa Kilimanjaro,” alisema.
Kadhalika Askofu huyo aliwaasa Watanzania kulinda amani na umoja wa taifa kwa nguvu zao zote na kamwe wasikubali kurubuniwa au kutenganishwa na watu wachache au kundi la watu kwa imani za kidini au itikadi za kisiasa.
Alisema watu wanapaswa kufahamu kuwa  amani ikitoweka, kuirejesha ni vigumu na ni gharama kubwa.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...