Sunday, November 11, 2012

Ndugu yangu, matusi, ngebe za nini katika mapenzi?

KUNA wanaume wanatukana matusi wake zao, yaani ukiwaona wanavyotukana unaweza ‘kufa’ kabisa. Huwezi kuamini kama ndio wale ambao walikuwa wanaitana ‘mpenzi’ nk.
Matusi ya nguoni, wakati mwingine kupigana hadharani au hata ndani mkiwa wawili ni dalili kwamba akili yako haiko sawa. Mwenye hekima hawezi kufikiria kumtukana mwenzi wake kama ndio jibu la kuimarisha uhusiano.
Je wewe ni kati ya wanaume ambao wamekuwa wakiwatukana wake zao? Je wewe ni kati ya wanaume ambao wake zao ni ‘ngoma’…kitu kidogo makofi? Kitu kidogo “rudi kwenu mbwa weeeee!”
Dalili kwamba wewe ni mwanaume mpumbavu, ni kuendekeza kutukana matusi au kutishana au kumwambia mwanamke rudi kwenu. Wazazi wako waliokuzaa sio kwamba hukuwakosea, lakini sifikiri kama waliwahi kusema wewe kuanzia leo si mtoto wetu kwa sababu umetukera hili na lile.
Kwanini panapokuwa na tatizo, jibu ni matusi? Mbona unakuwa mwanaume mjinga ndugu yangu? Mwanaume ni kichwa. Ni hekima zaidi kunapokuwa na matatizo, kuangalia nini cha kufanya ili kurekebisha matatizo, sio kutukana.
Wapo wanaume kwa mfano kakutwa na mwanamke mwingine, badala ya kuomba msamaha anatumia  jeuri na nyodo … ‘na utaondoka hapa!’ Ndugu yangu dharau zinatoka wapi? Kwani wanawake wote duniani wameolewa na wewe? Wanaume wako wengi na wala si kweli kwamba amekuwa nawe kwa sababu hakuna wanaume wengine, bali sijui ni mpango wa Mungu au wa shetani akakutana nawe.
Si vizuri kutoleana maneno ya dharau  na kuonekana kana kwamba mmoja ndio mwenye kujikomba zaidi na ndoa, mwingine ndio bosi. Raha ya ndoa ni pamoja na wanandoa kuoneana huruma, kwa kuacha kutoleana maneno machafu.
Wapo pia wanawake ‘choo’….midomo yao ni kama imewekwa nini, akianza kutukana, mtaa mzima watajua du kumbe baba fulani huwa anavaa kufuli lililotoboka…kumbe baba fulani ujeuri wake wote kwa nje ni bure, mkewe ndio mwenye kumsaidia. Siri zote za ndani zinatoka nje kana kwamba makaratasi yanapulizwa na kimbunga kikali.
Juzi nilikuwa nahojiwa na kituo cha radio cha Ufaransa, mtangazaji akawa anauliza kwanini hali ni mbaya katika ndoa? Jibu lake ndugu zangu ni rahisi, wengi wana nyodo, kujaliana kama wapenzi hakupo kwa baadhi ya watu.
Mapenzi ni kupeana raha sio kuwekeana masharti kama jela. Watu wanapoingia kwenye ndoa, matarajio yao sio kusaka watu wa kuwatukana matusi, wala kuwapiga, bali wanatafuta watu wa kushirikiana nao.
Kuna watu wanaona ni bora kukaa upweke kuliko kuingia katika uhusiano kutokana na hulka ya kuwekeana masharti. Wengine ni maarufu wa dhana…ukichelewa kurudi nyumbani anachojua ni kwamba ulikuwa kwa wanaume au wanawake.
Maisha ya dhana yanakera. Akikuona unaongea na simu, labda anakaribia na wewe ukawa umemaliza kuongea, anachofahamu ni kwamba ulikuwa unaongea na mpenzi mwingine, ndio maana umekata. Haya ni maisha ya kijinga.
Lakini pia ni ujinga kwa mtu kuwa mwenye uhusiano na kuanzisha uhusiano mwingine. Mtu ambaye ni mbaya, kwa maana ya kwamba ana uhusiano halafu anaanzisha na mwingine, kiasi kwamba simu yake inafungwa kwa namba fulani za siri, ana namba zake za siri ambazo mwenzi wake haruhisiwi kuingia kwenye mitandao yake ya kijamii, ni dalili mbaya na yenye kukera.
Ikiwa kwa mfano mwenzi wako ana simu, dalili kwamba si mwaminifu ni pale anapoifungia kwa namna za siri. Unaweza kumdanganya mwenzi wako kwa staili unazojua, lakini huo ni ukweli kwamba hiyo ni dalili mbaya.
Maana hakuna kazi ya siri kiasi cha kuzuia mwenzi wako asiijue. Hata ukiwa usalama wa taifa, huwezi kuoa, bila mwenzi wako kwa namna moja ama nyingine kujaza fomu fulani za kutambulika kwake na kwa kiasi kikubwa ni lazima atajua, kinyume na hicho hafai kuwa mke au mumeo. Kama humuamini mwenzi wako kiasi cha kuweka alama za siri kwenye e-mail, facebook nk, ni wazi kuwa hakufai huyo, una mwingine unayemjali na hakuna ubishi kwamba njia zako si safi.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...