Asema kifo chake ni pigo katika sekta za afya na elimu nchini
Rais Jakaya Kikwete akiweka shada la maua kwenye kaburi la Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.
Akizungumza katika ibada ya mazishi
iliyofanyika Ijumaa wiki hii alisema hayati Askofu Balina alikuwa
rafiki yake kwa siku nyingi na kuongeza kuwa kabla ya kifo chake
walikuwa wakiwasiliana kwa simu akiwa hospitalini Bugando.
Askofu Balina alifariki Jumanne wiki hii
katika hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza, baada ya
kusumbuliwa na saratani ya ini na kisukari.
Rais alikuwa akitoa salamu za serikali
katika ibada ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki la Mama
Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo mjini Shinyanga.
Pamoja naye alikuwepo Rais wa awamu ya
tatu Benjamin Mkapa na Mama Maria Nyerere, Mawaziri wa Mambo ya Nje
Bernad Membe na wa Ujenzi Dk. John Magufuli, wabunge , viongozi wa
dini na waumini.
Rais Kikwete alimsifu Balina kuwa tangu
alipopata upadirisho mwaka 1971 alikuwa kiongozi madhubuti wa kiroho,
asiyebagua na alikuwa mwadilifu katika shughuli zake .
Akieleza zaidi alisema Askofu huyo
aliisadia serikali katika masuala mengi yanayohusu afya na elimu huku
akishirikiana kutafuta wafadhili wa ndani na nje kwa kukisaidia Chuo
Kikuu cha Afya Bugando.
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Maaskofu
Tanzania (TEC), Mhashamu Askofu Tarsius Ngalalekumtwa, alisema kifo cha
Askofu Balina , kimewahuzunisha kwani alijitoa kwa ajili ya TEC na
kwa Watanzania .
Alisema Balina alikuwa Mwenyekiti wa
Idara ya Afya ya Kanisa Katoliki na Makamu Mwenyekiti wa Idara ya Fedha
ya Shirika la Maendeleo la Kanisa Katoliki (CARITAS).
Alimueleza kama kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kupamba na Ukimwi na mtumishi wa Jimbo la Shinyanga na taifa kwa ujumla.
Naye Mwakilishi wa Baba Mtakatifu
Francisco Padilia, aliwapa pole Wakatoliki wa Jimbo la Shinyanga na
Geita na kusema Baba Mtakatifu Papa Bendictor wa 16 amemteuwa Askofu
Mkuu wa Jimbo la Mwanza Thadeus Rwaichi kuwa msimamizi wa kitume wa
Jimbo la Shinyanga kwa sasa mpaka atakapomteua askofu mwingine.
No comments:
Post a Comment